1. UMUHIMU WA KUJIFUNZA NADHARIA ZA FONOLOJIA
UTANGULIZI
Kila linalofanywa na binadamu ili liwe ni lenye kufanikiwa linahitaji mwongozo ambao
utakuwa dira kwa jambo hilo. Mwongozo wa jambo lolote sharti uwe na vigezo ambavyo
vitawawezesha watu wengine kujifunza na kulifahamu jambo hilo. Kutokana na vigezo
hivyo, huwajengea utaratibu maalumu unaowawezesha na kuainisha ubora na udhaifu
unaojitokea katika jambo hilo.
Lengo la kazi hii ni kueleza umuhimu wa kujifunza nadharia mbali mbali za fonolojia.
Lakini kabla hatujajikita katika kiini cha swali ni vyema tukajikumbusha fasili ya
nadharia, ambapo neno hili ni istilahi ya msingi katika swali letu. Kwa mujibu wa
Massamba, D.P.B (2004:63) Nadharia ni kanuni na misingi ambayo hujengwa katika
muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kiolezo ya kueleza jambo.
Kwa mujibu wa fasili hiyo, tunapozungumzia neno nadharia tuna maana kwamba
nadharia ni maelezo ya jambo yaliyofungamana na vigezo vilivyowekwa au
vilivyozalishwa kutokana na uchunguzi uliofanywa. Vigezo hivyo ndivyo vinavyounda
kanuni na misingi ya kulieleza jambo lilokusudiwa. Nadharia kama mawazo, inaweza
kutokana na mtaalamu au kundi la wataalamu waliokaa na kufanya uchunguzi juu ya
jambo fulani.
Nadharia za fonolojia kwa ujumla wake ni mawazo ya wanaisimu kuhusu fonolojia za
lugha yaliyofungamana vigezo vilivyowekwa na wataalamu hao baada ya kufanya
uchunguzi. Nadharia za fonolojia ni mwongozo unaomwelekeza mwanaisimu chipukizi
au mtu anayejifundisha fonolojia, kuifahamu fonolojia ya lugha katika vipengele vyake
vyote. Kupitia mwongozo huu, mwanaisimu hujijengea utaratibu maalumu
utakaomwezesha kujua ubora na udhaifu utakaojitokeza katika nadharia nyengine.
UMUHIMU WA KUJIFUNZA NADHARIA ZA FONOLOJIA
1
2. Fonolojia kama tawi la isimu ni kongwe sana. Limeanza kufanyiwa kazi katika karne
nyingi zilizopita. Maendeleo hayo ya fonolojia yanaonesha kupita katika hatua kadhaa,
hatua ambazo zimejengwa kwa nadharia tofauti. Hivyo basi, kujifunza nadharia mbali
mbali za fonolojia ni muhimu kama ifuatavyo:-
Mosi, taaluma za fonolojia ni muhimu sana katika jamii yoyote ya lugha. Tawi hili la
isimu hujishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa sauti za lugha kisayansi.
Kutokana na umuhimu wa taaluma hii kwa jamii hatuwezi kuibeza. Njia mwafaka ya
zaidi ya kushughulikia somo la fonolojia kitaalamu ni kutumia nadharia. Hivyo kujifunza
nadharia ni muhimu kwa sababu tunapata kujua maumbile ya lugha tofauti ulimwenguni.
Mfano tunaweza kujua makundi ya lugha kama vile lugha zenye toni asilia, lugha zenye
viini toni, lugha zenye mkazo na lugha ambazo hazina toni wala mkazo.
Pili, nadharia za fonolojia humsaidia na kumuongoza mwanaisimu kuzibainisha kadhia
mbali mbali zinazozikabili kazi za wanaisimu wengine. Mfano, wanaisimu; Noam
Chomsky na Morris Halle walisoma kazi za fonolojia zilizoandikwa na akina Ferdinand
de Saussure, Bloomfield na wengine na kuona kuwa wanaisimu hao walitofautiana katika
kuzieleza sauti za lugha licha ya kuwa walieleza kitu kimoja. Kwa hivyo, Chomsky na
Halle wakaanzisha nadharia iliyojulikana kama Fonolojia Zalishi ili kujaribu kutatua
matatizo hayo.
Tatu, kujifunza nadharia mbali mbali za fonolojia huwasaidia wanaisimu chipukizi kuwa
mahiri na weledi katika uwanja wa fonolojia. Kwa sababu nadharia zinatoa mwongozo
unaowaelekeza wanaisimu kujua hatua mbali mbali za maendeleo zilizopitiwa katika
uwanja wa fonolojia. Kutokana na kujifunza nadharia mbali mbali mwanaisimu hupata
vigezo imara vinavyosaidia kutanua taaluma na maarifa aliyoyapata katika uwanja huu
wa fonolojia.
Nne, ni kawaida ya binadamu kudadisi kazi za wengine ili kuweka bayana ubora na
udhaifu wa uliomo katika kazi hiyo hasa inapokabiliwa na hali tete. Katika hali ya kuzua,
kuchuja na kukuza mikakati ya kutafitia , nadharia mpya inahitajika ili kuzilinda hoja
2
3. zake. Mfano, katika uwanja wa fonolojia, mwanaisimu John Goldsmith ilitafiti kazi ya
Fonolojia Zalishi iliyoandikwa na Chomsky na Halle na kubaini kuwa yapo matatizo
kadhaa yanayojitokeza wakati wa kuwakilisha vipambasauti kama vile mkazo, toni,
usilabi na unazali kwani vipengele vyote vya kifonolojia viliwakilishwa kwa mstari
mlalo. Ili kujaribu kutatua matatizo hayo, Goldsmith akanzisha nadharia mpya
iliyojulikana kama Fonolojia ya Vipandesauti Huru. Nadharia yake ilipendekeza
vipambasauti viwakilishwe kwa mistari mingi.
Tano, kujifunza nadharia mbali mbali za fonolojia ni muhimu kwa sababu hutuwezesha
kujua historia na maendeleo ya fonolojia katika vipengele mbali mbali. Kwa mfano
tunapata kuzijua nadharia za awali na waasisi wake. Matatizo yaliyojitokeza katika
nadharia hizo pamoja na kuzijua nadharia za sasa na namna zinavyojaribu kutatua
matatizo yaliyojitokeza katika nadharia za zamani. Mfano, kupitia nadharia za zamani
tunamjua mwanaisimu Trubetzkoy ambaye alianzisha nadharia ya fonimu. Wanaisimu
wengi wa sasa hawakubaliani na nadharia yake lakini hawawezi kuubeza mchango wake
katika maendeleo ya nadharia za fonolojia na sayansi ya isimu.
Kutokana na maelezo hayo, tunaweza kusema kuwa kujifunza nadharia mbali mbali za
fonolojia ni muhimu sana kwa wanafunzi wa lugha, wanaisimu na watumiaji wengine wa
lugha. kwa lengo la kubaini ubora na udhaifu wa nadharia ili tuweze kuzitumia nadharia
hizo kuchunguza, kuchambua na kuchanganua vipengele mbalimbali vya fonolojia.
Mwanaisimu anaejua nadharia mbali mbali za fonolojia huwa mahiri na mjuzi aliyebobea
katika kuvichambua vipengele mbali mbali vya fonolojia.
Pamoja na hakuna nadharia inayojitosheleza katika kiunzi chake. Hii ina maana kwamba
tunazo nadharia mbali mbali zinazohusu taaluma hii ya fonolojia lakini kila nadharia ina
ubora wake na udhaifu wake. Hivyo wanaisimu waendelee kufanya tafiti ili kuunda
nadharia mpya.
MAREJEO
Massamba,D.P.B (2004), Kamusi ya Falsafa ya Lugha na Isimu. Dar es Salaam
University Press.
3